
Taarifa
iliyotolewa leo December 11 2013 na Albert Msando ambae ni Mwanasheria
wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe kuhusu zile headlines za hivi
karibuni za kuvuliwa vyeo CHADEMA imesema ‘baada ya kupokea barua yake
ya mashtaka 11 tarehe 01/12/2013 ambayo anashitakiwa nayo na iliyomtaka
ajitetee kwa maandishi, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB) jana tarehe
10/12/2013 amefanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji
za Chama’
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB) ametoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa
Chama kumueleza nia yake kukata rufaa Baraza Kuu la Chama kupinga hatua
iliyochukuliwa na Kamati Kuu dhidi yake kumvua nyadhifa zake ndani ya
Chama ambapo kuna sababu mbili za msingi za kukata rufaa;
1. Utaratibu wa kuchukua hatua za nidhamu ulikiukwa. 2. Sababu za kuchukuliwa hatua hizo sio sahihi.
Utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za
kinidhamu kiongozi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji ni kama
ifuatavyo;
Kanuni ya Uendeshaji inasema kiongozi yeyote hatochukuliwa hatua za
kinidhamu bila kwanza kupewa mashitaka yake kwa maandishi na mamlaka
husika na kupewa nafasi ya kujibu mashitaka kwa maandishi pia tunapenda
ijulikane kwamba Kanuni ya Uendeshaji 6.5.2 (a), (b), (c) na (d) kama
ilivyorekebiswa Januari 2013 inasema;

Kwa
mujibu wa ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba mwanachama yeyote
hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama
kufukuzwa uanachama bila kwanza;
a) Kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.
b) Kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika.
c) Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa.
d)Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu
(b), (c) hapo juu kama itaona maslahi ya Chama kwa ujumla yanaweza
kuathiriwa isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika
kuitwa kwenye kikao husika.
Naomba nichkue fursa hii kufafanua kuwa uongozi wa chama ulifanya
mkutano na waandishi mnamo tarehe 26/11/2013 na kusema kwamba
marekebisho haya ya Kanuni ya mwaka 2013 ambayo nimewawekea hapo juu,
ndiyo utaratibu waliofuata pia walieleza kuwa sikuwa naifahamu na
nilidanganywa kwani Kanuni ilishabadilishwa.
Mabadiliko haya ambayo ni katika kipengele (d) kuhusu hatua ya
dharura iliyochukuliwa na Kamati Kuu haikugusa kipengele (a) cha Kanuni.
Yaani ni kuwa hata kama Kamati kuu itachukua hatua ya dharura kwa
mujibu wa kipengele (d), bado kipengele (a) ni lazima ifuatwe na
inatamka wazi sharti la kiongozi kupewa mashtaka kwa maandishi na kupewa
nafasi ya kujibu kwa maandishi. Hii ni haki ya msingi kwa kila utawala
au uongozi.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hakupewa mashtaka yake aliyakuta ndani
ya kikao baada ya kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu (text message au
sms) ambapo kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa uongozi na
kwa kuangalia athari zake kwake yeye binafsi na chama kwa ujumla,
Kamati Kuu ilitakiwa kujiridhisha kwamba Kanuni za Uendeshaji na Katiba
zinafuatwa.
Hili linaendana na utaratibu uliotumika kwa Samson Mwigamba kuvuliwa
nyadhifa yake ya uenyekiti wa mkoa. Yeye hakuitwa kabisa kwenye kikao
hicho na ni ukiukwaji wa Kanuni ya Uendeshaji
6.5.6(d) niliyoisoma hapo juu kwamba lazima kiongozi huyo aitwe
kwenye kikao, sababu zilizotumika ingawaje hajapokea taarifa rasmi ya
maandishi kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji ni kwamba yeye ameshirki
kwenye kuandaa na kusambaza waraka ambao unasemekana ni mkakati wa
ushindi wenye lengo la kupindua uongozi uliopo.
Waraka huo haukumtaja Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kama muandaaji au
msambazaji. Waliouandaa hawajaukana na badala yake wamesema waziwazi
kabisa kwa maneno na maandishi kwamba Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe
HAHUSIKI. Sio sawa kumuadhibu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kwa hisia au
tu kwa sababu ya urafiki wake na watu fulani.
Haya ni mapungufu ambayo kwa bahati nzuri Katiba na Kanuni za
Uendeshaji zinatoa nafasi ya kurekebishwa kwa kutoa nafasi ya kukata
rufaa. Na utaratibu ni huu hapa Kwa ufupi, Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya
Chama kwamba “Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake
ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake
ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”
Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama “Rufaa yoyote lazima ifanyike
katika muda wa siku thelathini tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa
maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa adhabu”
Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa ufuatwe ili
kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa
maneno haya, kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji >> “Kiongozi
aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu
ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”
Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji >> “Mwadhibiwa
atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku
thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabu”
Kanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji >> “Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa
taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu.
Taarifa hiyo lazima ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao
cha mamuzi”
Mpaka hivi sasa hatujapokea taarifa kamili ya mwenendo wa shauri
tokea kikao cha Kamati Kuu cha tarehe 20-21/11/2013 Huo ndio utaratibu
ambao Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ameamua kufuata kwa kuheshimu
maamuzi ya Kamati Kuu lakini kukatia rufaa maamuzi hayo. Kuheshimu
maamuzi sio kuyakubali uhalali wake.
Kumekuwa na matukio ya kusikitisha ambayo mengine yamefikia mahali
kuwa fujo na vurugu ikiwa ni pamoja na kurushiwa mawe Katibu Mkuu wa
Chama ambapo baadhi ya vurugu hizo zimehusishwa na Mheshimiwa Zitto
Zuberi Kabwe na baadhi ya watu.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hahusiki kwa njia yoyote na hayo
yanayoendelea na anayakemea na kuwashauri wanachama wote kuwa watulivu
na kuendelea kuwaheshimu viongozi wa kitaifa. Hatua zimeshachukuliwa
kukata rufaa na ni imani yake kwamba Baraza Kuu la Chama litatenda haki
kwa kupitia rufaa yake na kutoa uamuzi.
MILLARD AYO